Wamasai wampongeza Magufuli kwakupigania rasilimali Za Nchi

Arusha. Viongozi wa mila ya kimasai maarufu Laigwanan wilayani Monduli, wamempongeza Rais John Magufuli kwa kupigania rasilimali za nchi ili ziweze kuwanufaisha wananchi wote.

Viongozi hao walitoa kauli hiyo juzi wilayani Monduli Juu baada ya kumalizika kwa kikao cha mila kilichofanyika chini ya mti maarufu na mkongwe wa Olopon, mahali ambako Waziri mkuu wa zamani marehemu Edward Sokoine alisimikwa kuwa kiongozi wa mila.

Mwenyekiti wa viongozi hao, Ngiboli Ngilepoi alisema wakiwa viongozi wa mila wanampongeza kwa dhati Rais Magufuli kwa kuhakikisha rasilimali za taifa zinarudi mikononi mwa wananchi.

Alisema hawatakuwa nyuma katika juhudi za kumpongeza Rais Magufuli kwani kwa kiwango kikubwa amehakikisha anapambana na wezi wa rasilimali za taifa, kitendo ambacho ni cha kizalendo. “Kama viongozi wa mila tunampongeza Rais Magufuli kwa kazi nzuri anayofanya ya kuhakikisha anapigania rasilimali za taifa,” alisema Ngilepoi.

Njokota Lami ambaye naye ni miongoni mwa wazee wa mila, alisema wanampongeza Rais Magufuli kwa kuwasimamia watendaji wake kama mawaziri ambao wamekuwa wakihakikisha wanatatua kero za wananchi.

Alisema uamuzi uliofanywa na Waziri wa maliasili na utalii, Dk Hamis Kingwangalla wa kurejeshwa kwa mifugo ya wakazi wa Loliondo iliyokamatwa wilayani Serengeti ni wa kujali masilahi ya wanyonge.

Naye Loota Sanare alisema viongozi hao wamekutana chini ya mti huo wenye historia lukuki ambao uamuzi mwingi ndani ya jamii ya kimasai hufanyika.

Alisisitiza kuwa viongozi wa kimila na wafugaji wanampongeza Rais Magufuli kwa kuhakikisha anajali masilahi ya wanyonge na daima katika vikao vyao wataendelea kumuombea.

Naye Saibulu Olemariki alisema kitendo cha Rais Magufuli kupiga marufuku kusafirishwa kwa mchanga wa madini nje ni kitendo cha ushujaa ambacho hakikuwahi kufanywa na watangulizi wake.

Comments

Popular posts from this blog

Faida ya kutumia ganda la Ndizi mbivu

Kurudisha nguvu za kiume

HISTORIA: Ernesto Guevara