Raila Odinga kuongoza NASA kiharakati

Nairobi, Kenya. Kiongozi mkuu wa upinzani wa National Super Alliance (Nasa), Raila Odinga ameubadili muungano huo wa kisiasa kuwa “muungano wa kiharakati” ambao hautakuwa unawatambua wala kuheshimu viongozi wa Serikali ya Jubilee.

Odinga amesema hayo leo Jumatano Oktoba 25,2017 alipowahutubia wafuasi wake kwenye viwanja vya Uhuru Park, Nairobi siku moja kabla ya kufanyika uchaguzi wa marudio kwa Urais.

"Hatutaitambua Serikali ambayo haitakuwa imechaguliwa kwa kuzingatia Katiba,” amesema akimaanisha utawala wa Rais Uhuru Kenyatta.

"Hatutawaheshimu Uhuru, (Makamu wa Rais William) Ruto, wakuu wa mikoa, makamishna wa kaunti na wengine wote..." amesema Odinga.

Pia, amewataka Nasa kufanya maombi mbali na vituo vya kupigia kura au wabaki majumbani kwao kesho Alhamisi Oktoba 26,2017 Kenya itakapofanya uchaguzi aliouita wa kinafiki.

"Msishiriki uchaguzi huo wa maigizo," amesema Odinga. Amewaeleza wanachama kwamba, "Nendeni mshawishi kila mmoja asishiriki uchaguzi huo."

Tofauti na tamko la awali, amewataka wafuasi wake wasithubutu kuingia mitaani akionya kuwa Serikali imesambaza polisi kwa ajili ya “kuwaua”.

Odinga ametoa tamko hilo baada ya  Mahakama Kuu ya Kenya kuondoa kwa kiasi fulani giza lililozingira uchaguzi wa marudio kwa kura ya urais uliopangwa kufanyika kesho baada ya kutupilia mbali maombi ya kutaka uahirishwe ikisema haina mamlaka hayo kisheria.

Baada ya juhudi zote za kuzuia uchaguzi kukwama, Mwenyekiti wa IEBC, Wafula Chebukati amelitangazia Taifa kwamba uchaguzi huo utaendelea kesho kama ulivyopangwa.

Amesema kazi ya usambazaji makaratasi ya kupigia kura na vifaa vingine ilikuwa inaendelea vizuri.

Chebukati amesema vituo vya kupigia kura vitafunguliwa kesho Alhamisi Oktoba 26,2017 saa 12:00 asubuhi na kutakuwa na usalama wa kutosha.

"Hakikisho ambalo tume imepewa na mamlaka husika na vyombo vya usalama hasa kwa kuzingatia maendeleo yaliyofikiwa hadi sasa na tume, uchaguzi utaendelea kesho kama ulivyopangwa," amesema Chebukati alipozungumza na waandishi wa habari katika ofisi za IEBC zilizoko jengo la Bomas.

Jengo hilo ndilo lililotangazwa katika Gazeti la Serikali kwamba kitakuwa kituo cha kujumlishia matokeo.

Katika mkutano huo na waandishi wa habari, Chebukati aliongozana na makamishna wote watano kuthibitisha kwamba hakukuwa na mgogoro wowote ndani ya IEBC.

Kesi zatupwa

Katika kesi ya kwanza Mahakama Kuu, Jaji George Odunga alikosoa mchakato uliotumiwa na IEBC kuteua maofisa wasimamizi wa uchaguzi na manaibu wao akisema haukuwa halali kwa kuwa ulikiuka Sheria ya Uchaguzi.

“Walalamikiwa (IEBC) wameshindwa kuwasilisha orodha ya watu waliopendekezwa na vyama vya siasa na wagombea binafsi walau siku 14 kabla ya siku ya mwisho ya uteuzi wao kuwezesha kuwa na uwakilishi, kwa kufanya hivyo wajibu maombi walikiuka Kanuni ya 3(2),” alisema Jaji Odunga.

IEBC iliteua maofisa 290 na manaibu wao kwa ajili ya kusimamia uchaguzi wa marudio unaofanyika kesho. Hata hivyo, Jaji Odunga alikataa kutumia hoja hiyo kuahirisha uchaguzi huo akisema mbele yake hakuna maombi ya kusogeza mbele uchaguzi wa marudio hivyo hawezi kutoa amri kama hiyo.

Katika kesi ya pili, Jaji Chacha Mwita aliyekuwa anasikiliza maombi yaliyowasilishwa na mbunge wa zamani wa Kilome, Harun Mwau akitaka uchaguzi uahirishwe alisema korti hiyo kisheria haina mamlaka na uchaguzi wa Rais. Mwau alitaka mahakama isitishe uchaguzi huo ili uteuzi uanze upya.

Kesi ya tatu ni iliyofunguliwa Mahakama ya Juu na wanachama watatu wa asasi za kiraia wakitaka uchaguzi uahirishwe. Hata hivyo usikilizwaji wa kesi hiyo iliyofunguliwa jana kwa hati ya dharura ulikwama baada ya kukosekana akidi ya kutosha ya majaji.

Comments

Popular posts from this blog

Faida ya kutumia ganda la Ndizi mbivu

Kurudisha nguvu za kiume

HISTORIA: Ernesto Guevara