Naibu waziri atoa agizo hili kwa madiwani
Madiwani nchini wametakiwa kuainisha barabara zote zenye kipaumbele katika maeneo yao ili ziweze kuingizwa kwa urahisi kwenye mpango wa matengenezo.
Wito huo umetolewa mkoani Tabora na Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Mheshimiwa Elias Kwandikwa (Mb), wakati akikagua ujenzi wa barabara ya Kaliua-Urambo yenye urefu wa KM 28.
Pamoja na wito huo Mh. Kwandikwa amesema mapendekezo yao yawasilishwe katika kamati za maendeleo za Wilaya, Mikoa na bodi za barabara hatua ambayo itarahisisha utambuzi wa barabara hizo.
“Unakuta diwani analalamika kwamba barabara haijatengenezwa ama haifikiriwi kutengenezwa lakini ukija kufuatilia unakuta hakuna mahali popote ambapo taarifa za barabara hiyo kutengenezwa zimewasilishwa”, amesema Mhe. Kwandikwa.
Aidha naibu waziri amesisitiza kuwa umuhimu wa kupeleka mapendekezo hayo kutasaidia barabara hizo kutambulika na kuondoa malalamiko kwa wananchi na baadhi ya viongozi kwa kuwa zitaingizwa katika mipango ya ujenzi kwa wakati.
Comments
Post a Comment