Maagizo ya Polisi mchezo wa Yanga Na Simba
Jeshi la Polisi kanda maalumu ya Dar es salaam kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama limejipanga ipasavyo kuhakikisha mchezo kati ya YANGA na SIMBA utakaochezwa kwenye uwanja wa Uhuru unakuwa katika hali ya usalama.
Aidha limewataka wananchi wasiwe na wasiwasi wowote wa kiusalama na pia watupe ushirikiano wa kutoa taarifa kwa jambo lolote watakaloliona kuwa linaweza kuwa chanzo cha uvunjifu wa amani kwa kipindi chote watakapokuwa ndani au nje ya uwanja.
Uwanja utafunguliwa saa 08: 00 na mashabiki wanatakiwa kuwahi mapema ili kuepuka usumbufu unaoweza kutokea, tiketi hazitauzwa siku ya mechi hivyo mashabiki wanatakiwa kukata tiketi mapema, tiketi 23,000 zitauzwa kutokana na uwezo wa uwanja huo, hivyo kwa wale mashabiki watakaochelewa kukata tiketi wanashauriwa kuangalia mechi hiyo kupitia Television na kusikiliza Radio.
Jeshi la Polisi kanda maalumu ya Dar es salaam linawataka mashabiki wote wasiokuwa na tiketi kutofika uwanjani ili kuepusha usumbufu watakaoupata pia mashabiki wa pande zote mbili wanatakiwa kukaa katika sehemu zao maalumu watakazopangiwa,
Kutakuwa na askari wa kutosha ili kuhakikisha sehemu zote za mageti ya kuingilia watu wanapekuliwa na magari hayataruhusiwa kuingia ndani ya uwanja bali watu wanatakiwa kuyapaki nje ya uwanja.
Pamoja na hayo wananchi wanatakiwa kuwa watulivu katika kushangilia mechi hiyo, na kuepuka kufanya mambo yafuatayo:
• Kuingia na chupa za maji
• Kuingia na mabegi
• Kuingia na silaha ya aina yoyote
• Kupaki magari ndani ya uwanja
• Kukaa sehemu ambazo tiketi zao haziwaruhusu.
Comments
Post a Comment